Sangoma' akutwa akimiliki SMG, risasi nane


Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha

Mganga wa kienyeji, Zacharia Ngobeko (35),  amekamatwa na polisi mkoani hapa baada ya kukutwa akimiliki SMG na risasi nane kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 1 jioni, baada askari polisi kufanya msako nyumbani kwake na kukamata silaha hiyo ikiwa na risasi zilizokuwamo kwenye magazine.
Kamugisha alisema baada ya kumhoji, alidai silaha hiyo ilitumika kufanya mauaji mbalimbali yakiwamo ya kumuua, Mary Kashidye, Februari 8, mwaka huu, kwa kumpiga risasi kutokana na ugomvi wa kiwanja kati yake na Jumanne Maige.
Aidha, alisema mauaji hayo yalifanyika baada ya kukodiwa vijana wawili, Andrew Buteye (38) na Daudi Luchemela (40), kutekeleza mauaji hayo, kisha kurejesha silaha hiyo kwa mganga huyo.
Kamanda Kamugisha alisema silaha hiyo kupitia vijana hao ilitumika katika tukio la unyang’anyi wilayani Kahama baada ya kumpora Manyangu Mboje, Sh. Milioni 1.5, dukani kwake Februari 13, mwaka huu.
Hata hivyo, alisema baada ya kuwahoji watuhumiwa wote walikiri kuhusika na matukio hayo ya mauaji na unyang’anyi kwa kutumia SMG hiyo na kisha kuihifadhi kwa mganga huyo huku wakikiri kufanya matukio mengine mkoani Mbeya mwaka 2010 na 2012.
Alisema watuhumiwa hao, pia walikiri kufanya uhalifu wilayani Sengerema mkoa wa Mwanza 2014, kwa kupora Sh. milioni 39. Watuhumiwa wote wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wiki ijayo kujibu mashitaka yanayowakabili.

Comments