Skip to main content
Search
Search This Blog
JAMII LEO
HABARI, MICHEZO, MATUKIO, ,MAKALA ,BURUDANI ,DINI ,VIPINDI VYA REDIO/TV
Share
Get link
Facebook
X
Pinterest
Email
Other Apps
Labels
event
news
April 29, 2015
Hatimaye Mbunge David Kafulila atunukiwa tuzo ya mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu.
Na Waandishi wetu
Pichani ni Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila (Picha na mwandishi wa jamiileo tz.blogspot.com).
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, ametunukiwa tuzo ya kutambua harakati zake za kutetea haki za binadamu katika mazingira hatarishi nchini, likiwamo sakata la uchotwaji wa mabilioni ya fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow.
Alikabidhiwa tuzo hiyo jana ikiwa imepita takriban mwaka mmoja tangu aibue bungeni kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ya uchotwaji wa zaidi ya Sh. bilioni 200 kifisadi kwenye akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Kashfa ya akaunti hiyo ilihusisha baadhi ya maofisa waandamizi wa serikali, wakiwamo mawaziri, katibu mkuu wa wizara, aliyekuwa mwanasheria mkuu wa serikali (AG), viongozi wa dini na majaji.
Mbali na Kafulila, wengine waliotunukiwa tuzo kama hiyo, ni pamoja na waliokuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba (BMK); Salma Said na Adil Mohamed.
‘Wajumbe’ hao walitunukiwa tuzo hiyo kutokana na kuwa kati ya watu waliokuwa wakifuatiliwa na mtu asiyefahamika kutokana na kutuhumiwa kuipigia kura ya hapana katiba inayopendekezwa katika Bunge hilo.
Mwingine aliyetunukiwa tuzo kama hiyo ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Wafugaji Wanawake Loliondo, Maanda Ngoitick, ambaye alifikia kudhalilishwa kwa kuitwa kuwa siyo raia wakati akiwatetea wanawake wa jamii hiyo.
Tuzo hizo zilizo andaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) zilitolewa katika maadhimisho ya Siku ya Watetezi wa Haki za Binadamu Duniani, jijini Dar es Salaam jana.
Harakati zao hizo zimetambuliwa na Ripoti ya Hali ya Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania ya Mwaka 2014 iliyotolewa na THRDC jana.
Katika maadhimisho hayo, maonyesho ya mashirika, taasisi, wadau, watetezi, wanaharakati, kikiwamo Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Jukwaa la Katiba (Jukata) na Jumuiya ya Ulaya (EU) na Chama cha Albino Tanzania (TAS), yalizinduliwa.
Mgeni rasmi katika maadhimisho alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Tom Bahame Bahame, ambaye alisema tume yake imejipanga kuzishirikisha taasisi mbalimbali katika kuhakikisha maadili ya uongozi yanafuatwa.
Alisema pia itahakikisha haki ya kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na ushiriki wa wananchi katika mchakato wa upigaji kura katika uchaguzi mkuu, mwaka huu.
KAULI YA KAFULILA
Akizungumza na mwandishi wa habari baada ya kupokea tuzo hiyo, Kafulila alisema amefurahishwa kuona kazi aliyoifanya imetambuliwa, kuthaminiwa kitaifa na kimataifa, kwani ni mara chache watu wanaotetea haki za binadamu kutambuliwa.
Alisema tuzo hiyo imemuongezea kasi ya kuendeleza mapambano ya kutetea haki za binadamu licha ya kuwapo kwa changamoto katika harakati hizo.
“Nafurahi kuona kazi niliyoifanya imetambuliwa na jumuiya za ndani na nje. Tuzo hii itanifanya niendeleze mapambano zaidi katika kutetea wanyonge wa taifa hili,” alisema Kafulila.
Mratibu wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, alisema watetezi wa haki za binadamu wamekuwa wakikumbwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo kupigwa au kutishiwa na hata baadhi ya mashirika kufikia kufungiwa.
Alisema katika kuelekea kipindi cha uchaguzi mkuu wa mwaka huu, kutakuwa na matukio mbalimbali kutokana na asasi za kiraia kuwa watetezi wa wananchi.
“Kumekuwa na baadhi ya viongozi, ambao hawazikubali kazi zetu za utetezi wa haki za binadamu, nasisitiza waendelee kufanya kazi bila uoga ili kufikia malengo yao,” alisema Olengurumwa.
Kuibuliwa kwa kashfa ya kaunti hiyo, kulisababisha Kafulila kuingia kwenye malumbano makali yaliyowafikisha katika kutoleana maneno ya dharau na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, bungeni.
Maneno hayo ya dharau yalihusisha Jaji Werema kumwita Kafulila kuwa ni tumbili na Kafulila kumwita Jaji Werema mwizi.
Kafulila alipoibua wizi wa fedha hizo viongozi kadhaa wa serikali walipinga wakisema kuwa ni mwongo hadi Bunge lilipoagiza uchunguzi ufanywe na Ofisi ya Mdhibiti Mkuu na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Pipoti ya uchunguzi huo wa CAG iliwasilishwa na Kamati ya Hesabu za serikali (PAC) iliyokuwa ikiongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe na baada ya kuipitia iliwasilishwa bungeni na kuwataja baadhi ya maofisa waandamizi wa serikali, wabunge, majaji na viongozi wastaafu kuhusika.
Ripoti hiyo ilisababisha aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka kufukuzwa kazi baada ya kubainika kupokea mgawo wa Sh. bilioni 1.6 kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya VIP Engineering and Markating LTD, James Rugemalira.
Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Jaji Frederick Werema alijiuzulu kutokana na kuishauri vibaya serikali wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, alisimamishwa kazi hadi uchunguzi dhidi yake utakapokamilika.
Naye aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Prof. Sospeter Muhongo, alijiuzulu wadhifa huo.
Wengine ni Mbunge wa Bariadi, Magharibi, Andrew Chenge na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja, waliondolewa katika nyadhifa zao za uenyekiti wa Kamati za Bunge za Bajeti na Katiba, Sheria na Utawala. Chenge alipokea Sh. bilioni 1.6 na Ngeleja Sh. nilioni 40 kutoka kwa Rugemalira.
Maofisa wengine wanakabiliwa na kesi mahakamani na wengine walihojiwa na Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.
Pia unaweza kujipatia habari na matukio mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kwa kulike page yetu katika ukurasa wetu wa facebook www/facebook.cm/jamiileo tz
CHANZO: NIPASHE
Comments
Popular Posts
March 12, 2013
USWAHILINI KUNA MAMBO ANGALIA PICHA HIZI ZA KANGA MOKO...SHETANI TOKAAAAAAAA!!!!!!
March 12, 2013
UNATAKA KUONA KANGA MOKO LAKI SI PESA...PICHA -- INYE NJE NJE...BALAA
Comments
Post a Comment