Soma taarifa kamili ya kifo cha Mbunge wa jimbo la Ukonga jijini Dar es salaam
Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Eugene Mwaiposa.
Mbunge wa Jimbo la Ukonga, Eugene Mwaiposa, amefariki dunia ghafla usiku wa kumamkia jana akiwa nyumbani kwake amelala.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliliambia Bunge jana kuwa Mwaiposa alikuwa na tatizo la shinikizo la damu kwa muda mrefu.Kufuatia kifo hicho aliahirisha kikaio cha Bunge kesho na kusema
kuwa mwili wa marehemu umepelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Mkoa
wa Dodoma kwa uchunguzi zaidi.
Ndugai alisema shughuli za kuaga mwili wa marehemu zitafanyika leo
mjini hapa baada ya familia yake kuwasili ikitokea Dar es Salaam.
“Taarifa nyingine tutazitangaza baadaye kupitia taarifa za mtandao
wa simu kuelezea taratibu za usafiri na mambo mengine,” alisema.
Alitangaza taarifa hiyo ya kuhuzunisha na kuwafanya baadhi ya
wabunge kububujikwa machozi kwa simanzi wakati wabunge wakijadili bajeti
ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kipindi cha mchana, mjadala ambao
ulikuwa ukiongozwa na Mwenyekiti, Lediana Mng’ong’o. Mng’ong’o alizamika kukatisha uchangiaji wa wizara hiyo ambayo
ilitakiwa kupitishwa jioni jana na kuwaambia wabunge kuwa Naibu Spika
ana taarifa anayotaka kuitangaza.
Mwaiposa hadi juzi jioni alionekana katika viwanja vya Bunge na kantini na Jumamosi alichangia bajeti ya Wizara ya Uchukuzi.Mwaiposa anafanya idadi ya wabunge waliofariki dunia mwaka huu kuwa
wawili baada ya Mbunge wa Mbinga Mashariki, John Komba, kufariki dunia
Machi, mwaka huu kwa shinikizo la damu.
Kifo cha ghafla cha Mwaiposa kimewashtua wabunge ambao muda mfupi
baada ya kuahirishwa Bunge walijikusanya kwenye makundi wakiwa na
huzuni, huku wakielezea jinsi wanavyomkumbuka wakati wa uhai wake.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti kwenye viwanja vya
Bunge, Mbunge wa Iramba Magharibi, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha,
Mwigulu Nchemba, alisema CCM imepoteza kiongozi mzuri ambaye alikuwa
akihudhuria vikao vya Bunge bila kukosa . Mwigulu alisema marehemu Mwaiposa kabla ya kufanyika uchaguzi ndani
ya chama alikuwa Mweka Hazina wa CCM Wilaya ya Ilala na kuongeza kuwa
chama kitamkumbuka kwa uchapaji kazi wake.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba,
alisema amepokea kifo cha Mwaiposa kwa mshtuko mkubwa na kwamba kabla ya
kufikwa na mauti hayo alizungumza naye kuhusu mpango wa serikali kutaka
kuligawa Jimbo la Ukonga.Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alisema
atamkumbuka Mwaiposa kutokana na michango yake aliyokuwa akiitoa katika
wizara hiyo.
“Juzi (Jumapili alishiriki semina ya mama afya na mtoto na
kuchangia, alikuwa Mbunge ambaye alikuwa karibu sana na wizara yangu na
kutoa ushauri mbalimbali,” alisema Dk. Rashid. Mbunge wa Viti Maalum
Mkoa wa Mbeya, Dk. Mary Mwanjelwa, alisema Bunge limepoteza kiongozi
makini na kwamba juzi alitaka kuchangia hoja katika Wizara ya Elimu na
Mafunzo ya Ufundi lakini aliahirisha kwa sababu ambazo hazikujulikana.
Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk. Faustine Ndungulile, alisema kifo
cha Mwaiposa kimekuja kipindi kibaya wakati bado alikuwa na mpango wa
kugombea jimbo hilo kuendelea kuwatumikia wananchi. Mbunge wa kuteuliwa
na Rais, James Mbatia, alisema atamkumbuka Mwaiposya kutokana na
misimamo yake ya kutoyumba katika jambo aliloliamini.
Alisema marehemu Mwaiposa alikuwa ni kiongozi ambaye hapendi
kushiriki siasa za kuchafuana na badala yake alitambua jukumu la mbunge
ni kutetea taifa, chama chake na wapiga kura wake.Mwenyekiti wa Bunge, Lediana Mng'ong'o ambaye ni Mbunge wa Viti
Maalum Mkoa wa Iringa, alisema mara ya mwisho marehemu alichangia
mjadala katika bajeti ya Wizara ya Uchukuzi.
Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko (Chadema), alisema taarifa za
kifo cha Mbunge huyo zilitolewa na dereva wa marehemu Mwaiposa baada ya
kufika nyumbani kwake Chadulu mjini Dodoma kwa ajili ya kumchukua
kumpeleka bungeni.
“Dereva wa Mheshimiwa Mwaiposa alipofika katika nyumba anayoishi
baada ya kugonga mlango na kuona hafungui, alikwenda kutoa taarifa Ofisi
za Bunge ndipo polisi walipokwenda eneo la tukio kuvunja mlango na
kukuta amefariki,” alisema.
Maganga Mkuu wa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Ezekiel Mpuya,
alisema mwili wa marehemu ulipokelewa saa 5:30 asubuhi na umehifadhiwa
katika chumba cha kuhifadhia maiti na wanasubiri maelekezo kutoka Ofisi
za Bunge kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi.
CHANZO:
NIPASHE
Comments
Post a Comment