Siku ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari
Ulimwengu unaadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani.
Maadhimisho hayo yanafanyika mjini Helsinki, Finland yakiongozwa na
shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO.
Ni siku ambayo dunia inatathmini hali ya uhuru wa vyombo vya habari
duniani kote, ambapo inatolewa michango ya kutetea vyombo vya habari
vinavyokabiliana na mashambulizi pamoja na kuwakumbuka waandishi habari
waliopoteza maisha yao wakiwa kazini.
Kila mwaka zaidi ya maadhimisho 100 ya kitaifa yanafanyika kuiadhimisha
siku hii. Na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa
UNESCO ndilo linaloongoza maadhimisho hayo katika kila pembe ya dunia.
Kauli mbiu ya siku hii kwa mwaka huu ni "upatikanaji wa habari na uhuru
wa kimsingi."
Uhuru wa Habari na Malengo ya Maendeleo Endelevu
Katika taarifa ya UNESCO iliyochapishwa kwenye tovuti yao,
Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Irina Bokova amesema:"Mwaka 2015 dunia
ilipitisha malengo 17 ya maendeleo endelevu. Ili kuhakikisha kunafanyika
juhudi zaidi katika miaka 15 ijayo za kukomesha umaskini, kuhakikisha
ustawi kwa wote, kuilinda dunia, pamoja na kuendeleza amani. Tunaweza
kufikia malengo hayo iwapo tutafanya kazi kwa pamoja na kama tutakuwa na
taarifa zenye ubora. Kutokana na hayo ndio maana siku ya uhuru wa
vyombo vya habari ya 2016 inayozinduliwa mjini Helsinki, imeamua
kuonyesha umuhimu wa uandishi wa habari ulio huru katika kutekeleza
ajenda ya maendeleo endelevu yanayotegemewa kutekelezwa ifikapo mwaka
2030."
Shirika la UNESCO pamoja na serikali ya Finland wanashirikiana kuandaa
sherehe kuu ya siku ya leo pamoja na sherehe ya tuzo ya UNESCO ya
Guillermo Cano kwa mwaka 2016, zitakazofanyika kwa pamoja katika mji
mkuu Helsinki na zinategemewa kumalizika tarehe 6.
Tuzo ya Guillermo Cano kwa Mwandishi habari wa Azerbaijan
Khadija Ismayilova, mwandishi wa habari za uchunguzi kutoka
Azerbaijan, ndiye aliyechaguliwa kupokea tuzo ya mwaka huu ya Guillermo
Cano ya UNESCO.
Ismayilova, ni mwandishi wa kujitegemea na mchangiaji wa idhaa ya
Azerbaijani ya Radio Huru ya Ulaya. Desemba mwka 2014 aliwekwa kizuizini
na Septemba 2015, alihukumiwa kifungo cha miaka saba na nusu kwa tuhuma
zinazohusiana na matumizi mabaya ya madaraka na ukwepaji wa kodi.
Tuzo hiyo ilianzishwa kwa mara ya kwanza na Halmashauri Kuu ya shirika
la UNESCO mwaka 1997. Na hafla hiyo ya kila mwaka inatoa tuzo ya heshima
kwa mtu, shirika au taasisi yoyote ambayo imechangia pakubwa katika
masuala ya utetezi na, kukuza uhuru wa vyombo vya habari mahali popote
duniani
Halikadhalika siku hii ya kimataifa ilitangazwa katika Mkutano Mkuu wa
Umoja wa Mataifa wa mwaka 1993 kufuatia pendekezo liloyopitishwa katika
Kikao cha 26 cha Mkutano Mkuu wa UNESCO wa mwaka 1991.
Siku ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu inaonyesha uhusiano kati ya
uhuru wa vyombo vya habari, utamaduni wa kuwepo kwa uwazi na haki ya
uhuru wa habari, na maendeleo endelevu katika karne ya mawasiliano ya
digitali. Suala moja muhimu katika haya yote ni jukumu la uandishi wa
habari, na umuhimu wa kuwalinda wale ambao wanahusika na taaluma hii
inayohudumia umma kwa kuwaletea habari zinazoendelea duniani kote.
Mwandishi: Yusra Buwayhid
Mhariri:Yusuf Saumu
Comments
Post a Comment